Hi Comrades!
Leo nawaletea makala niliyoitoa mwishoni mwa Desemba kuhusu East Africa Community/Federation. Hii ni sehemu ya kwanza, I hope it will be educative.
Karibuni...
Dk Nangale: Mchakato wa Shirikisho wahitaji mijadala ya kina na muda zaidi
MIONGONI mwa mambo ambayo yameshika kasi wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ambayo Desemba 21 mwaka huu ilitimiza mwaka mmjoa tokea iingie madarakani ni suala la kuharakisha ushirikiano wa kisiasa wa Afrika Mashariki (Shirikisho). Suala ambalo bado halijapata udadavuzi wa kina ni kuhusu kwanini tuwe na haraka ya kufikia Shirikisho? Imepangwa kuwa ifikapo mwaka 2013, nchi za Afrika Mashariki ziungane na kuwa nchi moja katika mfumo wa Shirikisho kwa maana ya kuwa pamoja na kwamba kila nchi itakuwa na Rais wake, Serikali yake, Bunge lake na Mahakama zake, lakini nchi hizo ziunganishwe katika mwamvuli mmoja wa Afrika Mashariki ambao utakuwa na Rais wa Afrika Mashariki, Bunge la Afrika Mashariki na Mahakama ya Afrika Mashariki sambamba na kulifanya eneo hilo kuwa ni eneo moja la kibiashara linalotambulika kimataifa. Katika makala hii, mwandishi HAWRA SHAMTE anazungumza na mbunge mkongwe wa Bunge la Afrika mashariki na ambaye pia ni Mwenyektii wa kamati ya Mawasiliano Biashara na Vitega uchumi katika Bunge la Afrika Mashariki, DK GEORGE NANGALE ambaye analieleza kwa kina chimbuko la kuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, muundo wake, taratibu zake na makubaliano yaliyofikiwa. Kadhalika Dk. Nangale anajibu swali la kwanini kuharakisha Shirikisho?
“Tulipoanzisha upya Jumuiya ya Afrika Mashariki, miaka 10 iliyopita, tutakumbuka kwamba ilitokana na azimio lililotolewa baada ya kuvunjika ile ya zamani. Sasa wakati wanajaribu kukusanya na kugawana zile rasilimali zilizokuwapo wakaona kwamba siyo kitu cha busara kufuta kabisa kila kitu. Kwa hiyo kuna taasisi zilibaki, kama vile East African Development Bank na taasisi nyingine kama zile za utafiti. Lakini vilevile yakatokea mawazo kwamba siku zijazo ni vizuri tuangalie upya namna gani tutaweza kushirikiana, kwa hiyo wale marais waliokuwapo wakati ule, Rais Daniel Arap Moi, Rais Ali Hassan Mwinyi na Rais Yoweri Museveni waliangalia jinsi ya kuifufua Jumuiya ya Afrika mashariki. Walipokubaliana hivyo, mwaka 1996 wakasema kwamba wananchi waanze kujadili, kuona waunde jumuiya ya aina gani. Yakaanza majadiliano katika nchi hizo tatu, majadiliano yale yalishirikisha Serikali na Wadau, yalichukua miaka minne,” anasema Dk.George Nangale.
“Kwa kuwa kulikuwa na mawazo kwamba pengine ni vizuri kuunda jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Mashariki, wadau kama wafanyabiashara, Jumuiya za kijamii, wasomi na Serikali walianza kujadili suala hilo. Kwa hiyo kulikuwa kuna mjadala kaunzia 1996 mpaka 1999. Ilipofika Novemba 1999, wataalam wetu, wanasheria wakuu na wabunge walipata nafasi ya kulijadili suala hilo kwa undani kwamba je tunaanzisha jumuiya ya aina gani?
“Novemba 30 , 1999 ukasainiwa mkataba (Treaty for the Establishment of East African Community) viongozi wakakubaliana kuwa utaanza rasmi kazi zake Julai mosi 2000. mkataba ule umejikita katika mambo makuu matano, kwanza muundo, je tutakuwa na muundo wa aina gani?
Muundo wa Jumuiya:
“Makubaliano yakawa kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na asasi (organs) mbalimbali ambazo zitasaidia kusukuma mbele azma ya jumuiya yenyewe. Hivyo tukakubaliana kwamba kutakuwa na Sekretarieti na Arusha itakuwa ndiyo makao makuu ya jumuiya. Sekretarieti itasimamia shughuli za kila siku za jumuiya, pia tukakubaliana kuwa kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo kazi yake itakuwa ni kusimamia sera. Ilionekana kwamba kazi kubwa ya Jumuiya ni kuainisha na kuziweka sawa sera zetu kwa sababu tutakuwa na sera zinazotofautiana,” anasema Dk. Nangale.
“Asasi ya tatu ni Bunge, kwamba tutakuwa na Bunge la Afrika Mashariki ambalo kazi yake kubwa itakuwa ni kutunga sheria ambazo zitakuwa zinaongoza masuala yote ambayo tutakubalina wkamba tutayafanya kwa pamoja, siyo kutunga sheria zote ila kuhusu yale mambo tuliyokubaliana kwa wakati huo.
“Asasi nyingine ni Mahakama ya Afrika Mashariki. Mahakama hii si mahakama ya rufaa, ni mahakama ambayo kimsingi inatafsiri uhusiano wetu kwa maana ya kutafsiri katiba. Kama kuna tofauti zozote za utekelezaji wa katiba au masuala tuliyokubaliana, mahakama itakuwa inaingilia kati kutoa ufafanuzi na kutoa mapendekezo kwamba hili limefanyika sawa au siyo sawa.
“Asasi nyingine ni ‘Summit,’ Wakuu wa Nchi. Hawa watakutana katika Baraza lao la Wakuu wa Nchi, hawa ndio wasimamizi wakuu wa shughuli zote za Jumuiya. Kazi yao moja ni kuridhia yale tuliyoyapitisha bungeni na ni lazima marais wote waridhie ndipo suala hilo litakapopita. Kwa hiyo Summit ndiyo asasi ya juu zaidi kuliko asasi zote za Afrika Mashariki.”
Misingi ya Ushirikiano (The Principle of Cooperation):
Shabaha yetu ilikuwa ni kutoka kwenye ushirikiano mdogo (Cooperation) kwenda kwenye mahusiano makubwa (Integration). Ili tufanye hivyo kuna misingi mitatu tuliyokubaliana.
Msingi wa kwanza ni ‘Principle of Subsidiarity’;
Ni msingi ambao tunakubaliana kwamba katika ushirikiano wetu hatuwezi tukashirikiana katika kila kitu, kuna baadhi ya mambo tutashirikiana na baadhi ya mambo hatuwezi kushirikiana. Kwa hiyo tutashirikiana katika masuala fulani fulani ambayo tunadhani kwamba tunaweza tukashirikiana kwa ridhaa ya nchi zenyewe.
Msingi wa pili ni ‘Principle of Variable Geometry’;
Ni msingi ambao unatambua kwamba nchi zetu ziko tofauti, kiuchumi, kisiasa, kimuundo na masuala mengi ambayo yako tofauti, kwa hiyo tunakubali kwamba asasi mbalimbali zilizomo ndani ya hizi nchi zitashirikiana kwa sasi zao na utaratibu wao. Kwa mfano jumuiya za wakulima labda zinakwenda taratibu kuliko zile za wafanyabiashara, kwa hivyo zitakwenda kwa kasi tofauti na misingi tofauti.
Msingi wa tatu ni “Principle of Assemetry’
Msingi huu unasema kwamba iwapo A ni sawa na B siyo lazima B iwe sawa na A. Maana yake ni kwamba kwa kutambua tofauti zetu siyo lazima nchi moja inavyoifanyia nchi nyingine kwamba ni lazima nchi hiyo nayo ifanye hivyo hivyo. Kwa mfano msingi huu umefanyiwa kati katika ushirikiano wa forodha, kwamba Tanzania itapeleka bidhaa zake Kenya bila ushuru kwa sasa hivi, wakati Kenya tutawatoza ushuru ili kujipa muda wa kujirekebisha kwa muda wa miaka mitano.
Namna ya kufikia maamuzi:
“Tulikubaliana katika Afrika Mashariki kwamba makubaliano yote yatafikiwa kwa pamoja. Kama limekuja jambo ambalo linataka maamuzi, ni lazima nyote mukubali, yaani nchi zote tatu zikubali. Hivyo tulikubaliana kwamba maamuzi yote ya Afrika Mashariki yatafanywa kwa ‘consesus’ kwa maana ya kwamba, Baraza la Mawaziri likikutana, Wakuu wa nchi wakikutana, kama mmoja atatofautiana na wenzake ina maana kwamba hilo suala litaendelea kujadiliwa, kwa hiyo majadiliano yataendelea mpaka wote wakubaliane, kwa hiyo ukisikia maamuzi yametolewa ya Afrika Mashariki ujue kwamba wote wamekubaliana, hakuna suala la kura bali makubaliano ya pamoja.
Awamu za utekelezaji wa makubaliano:
Tulikubalina kuhusu mahusiano yetu yaendeje, tulikubaliana kwamba tutakwenda hatua kwa hatua. Tulikubaliana kuwa kitu cha kwanza tutakachoanza nacho ni umoja wa ushuru wa forodha (Customs Union). Kwa sababu ilionekana kwamba uhusiano wetu mkubwa ambao ni lazima tuuimarishe ni ule wa kibiashara, ili kuwapa watu wetu masoko na kuinua maisha yao kupitia biashara.
Kwa hivyo tuliamua tuwe na awamu za mashirikiano, tukianzia na Umoja wa Ushuru wa Forodha. Suala la ushuru wa Forodha lilianza kujadiliwa tokea mwaka 1999 hadi 2004, protokali ikasainiwa Machi, 2004 na Bunge tukapitisha sheria ya Ushuru wa Forodha Desemba 2004 na ikaanza kutumika Januari 2005.
Awamu ya pili ni kuanzisha Soko la Pamoja (Common Market), majadiliano yake yameanza Julai mwaka huu na yataendelea mpaka 2008. Soko la pamoja linajumuisha pia masuala ya uhamiaji (free movement of people), masuala ya ajira, masuala ya kufanya biashara kwa pamoja yaani eneo moja la kibiashara duniani (East Africa is a single destination), kuwa na sheria zinazofanana, kuwa na sera zinazofanana hususan zile za kazi, kwamba tukiwa na sheria na sera zinazofanana za kazi, watu wetu wanaweza wakafanya kazi katika hizi nchi bila matatizo, tuwe na pasi za kusafiria za Afrika Mashariki na pia tuwe na vitambulisho.
Awamu ya tatu ni kuwa na Sarafu ya Pamoja (Single Currency/Monetary Union)
Majadiliano yalipangwa yaanze mwaka 2009 hadi 2011, hapo ndipo tuwe na Sarafu moja. Mwisho kabisa, baada ya kupitia awamu zote hizo ndipo tutakwenda kwenye Ushirikiano wa Kisiasa (Political Federation).
Mkataba uliposainiwa mwaka 1999 kulikuwa kuna makubaliano kwamba Afrika Mashariki itakwenda kwa awamu mpaka kufikia Federation, haikupangwa ratiba ya Federation kwa wakati huo, tulikubaliana kwamba tukimaliza awamu moja tutakwenda nyingine. Kwa mfano Ushuru wa Pamoja wa Forodha ilikuwa ni awamu ambayo ilipaswa kufanyiwa kazi kwa miaka mitano toka 2005 hadi 2010. Halafu majadiliano ya Soko la Pamoja yanaanza, na labda itaanza kufanya kazi mwaka 2009 hadi miaka mitano, baada ya hapo Sarafu ya Pamoja, majadiliano yanaweza yakaanza mapema lakini utekelezaji wake ukafanywa baadaye. Baada ya hapo ndio tuingie katika Shirikisho la Kisiasa.
Jumuiya ya watu
Makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1999 katika kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki tulikubaliana kuwa tuunde jumuiya ya watu. Jumuiya ya mwanzo iliyovunjika ilikuwa ni ya Serikali (more inter-governmental). Sasa hii tunataka iwe ya watu (people centered), kwa hiyo watu washirikiane katika hatua mbalimbali na asasi mbalimbali. Pamoja na kuwa Serikali ni wadau lakini hata sisi wananchi pia ni wadau. Kwa hivyo hata sekta binafsi na asasi za kijamii zitapewa nafasi katika Jumuiya hii mpya ya Afrika Mashariki.
Kwanini haraka ya kwenda kwenye ushirikiano wa kisiasa?
“Miaka miwili iliyopita Rais Benjamin Mkapa, Rais Museveni na Rais Mwai Kibaki walikutana Nairobi katika mkutano wa dharura. Kulikuwa kuna ajenda kwamba kwani ni lazima awamu zilizopangwa kufikia Ushirikiano ni lazima ziende kwa utaratibu huo? Haiwezekani kuziharakisha? Wakaunda Tume kujadili suala hilo, wakaunda Tume ya Wako ambayo ilizunguka na kukutana na wadau mablimbali, wabunge, wananchi, wafanyabiashara na ilifanya kazi kwa muda wa miezi sita. Ilipotoa ripoti yake, ile Tume ikasema kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wako tayari kuharakisha muungano wa Afrika Mashariki na ikatengeneza ratiba kwamba ifikapo mwaka 2010 tuwe tumeshafikia hatua fulani, 2012 tuwe na kura ya maoni na 2013 hizi nchi ziwe zimeshaungana kisiasa,” anasema Dk. Nangale.
“Hiyo haina maana kwamba hatua za kufikia Ushirikiano wa kisiasa zitafutwa, la hasha, bali awamu zote zitaharakishwa ama zitatekelezwa kwa pamoja.
Ripoti ile ikapelekwa kwenye mabunge ikajadiliwa. Bunge la Uganda waliizungumza, Bunge la Kenya wabunge walisomewa tu lakini hawakuizungumza rasmi, Bunge la Tanzania haikuizunguza rasmi ripoti ile. Katika Bunge la Tanzania ripoti ile ilizungumzwa kwenye semina ya wabunge, wabunge wengi waliikataa ripoti ile, lakini haikuzungumzwa katika kikao rasmi cha Bunge.
Katika Bunge la Afrika Mashariki ripoti ile ilipelekwa ingawa haikujadiliwa rasmi. Wakuu wa nchi walipopata ile ripoti wakakubaliana kuunda kamati za kuendesha mijadala, ili wananchi wapate nafasi ya kutoa maoni. Kila nchi ikaunda kamati, kamati hizo zimepewa miezi minane ya kukusanya maoni ya wananchi. Itakapofika Mei mwakani wanapaswa kuiwasilisha ripoti yao kwenye Baraza la mawaziri.
Lakini cha ajabu ni kwamba kwa upande wa Tanzania ndio kwanza inajiweka sawa katika kazi ya kukusanya maoni? Imesalia miezi minne tu Kamati hiyo inapaswa iwasilishe ripoti yake.
Monday, January 22, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment