Dk Nangale: Tuiweke nyumba yetu katika hali nzuri kabla ya kukaribisha wageni
MIONGONI mwa mambo ambayo yametiliwa kasi katika mwaka uliopita wa 2006 ni mchakato wa haraka wa kuelekea Shirikisho la Afrika Mashariki (fast trucking).
Wiki iliyopita mbunge wa Afrika Mashariki Dk. George Nangale alielezea umuhimu wa kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki na makubakubaliano ya mchakato wa kuelekea kwenye shirikisho. Kuhusu mpango kasi kuelekea Shirikisho, Dk Nangale anasema kuwa yeye haoni sababu za kuufanya mchakato huo polepole sana wala haraka sana, unaweza ukafikiwa kwa taratibu zake za kawaida kama ilivyokubaliwa awali. Hii ni sehemu ya pili ya mahojiano baina ya mwandishi HAWRA SHAMTE na Dk Nangale kuhusu mchakato wa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Swali: Kwanini haraka ya kwenda kwenye Shirikisho?
Jibu: Miaka miwili iliyopita Rais Benjamin Mkapa, Rais Museveni na Rais Mwai Kibaki walikutana Nairobi katika mkutano wa dharura. Kulikuwa kuna ajenda kwamba kwani ni lazima awamu zilizopangwa kufikia Ushirikiano ni lazima ziende kwa utaratibu huo? Haiwezekani kuziharakisha? Wakaunda Tume kujadili suala hilo, wakaunda Tume ya Wako ambayo ilizunguka na kukutana na wadau mablimbali, wabunge, wananchi, wafanyabiashara na ilifanya kazi kwa muda wa miezi sita. Ilipotoa ripoti yake, ile Tume ikasema kwamba wananchi wa Afrika Mashariki wako tayari kuharakisha muungano wa Afrika Mashariki na ikatengeneza ratiba kwamba ifikapo mwaka 2010 tuwe tumeshafikia hatua fulani, 2012 tuwe na kura ya maoni na 2013 hizi nchi ziwe zimeshaungana kisiasa. Hiyo haina maana kwamba hatua za kufikia Ushirikiano wa kisiasa zitafutwa, la hasha, bali awamu zote zitaharakishwa ama zitatekelezwa kwa pamoja.
Ripoti ile ikapelekwa kwenye mabunge ikajadiliwa. Bunge la Uganda waliizungumza, Bunge la Kenya wabunge walisomewa tu lakini hawakuizungumza rasmi, Bunge la Tanzania haikuizunguza rasmi ripoti ile. Katika Bunge la Tanzania ripoti ile ilizungumzwa kwenye semina ya wabunge, wabunge wengi waliikataa ripoti ile, lakini haikuzungumzwa katika kikao rasmi cha Bunge.
Katika Bunge la Afrika Mashariki ripoti ile ilipelekwa ingawa haikujadiliwa rasmi. Wakuu wa nchi walipopata ile ripoti wakakubaliana kuunda kamati za kuendesha mijadala, ili wananchi wapate nafasi ya kutoa maoni. Kila nchi ikaunda kamati, kamati hizo zimepewa miezi minane ya kukusanya maoni ya wananchi. Itakapofika Mei mwakani wanapaswa kuiwasilisha ripoti yao kwenye Baraza la mawaziri.
Swali ni je Kamati ya kukusanya maoni kwa upande wa Tanzania tayari imeshaanza kazi ya kukusanya maoni? Imesalia miezi minne tu Kamati hiyo inapaswa iwasilishe ripoti yake.
Swali: Je kuna changamoto gani zinazoikabili Jumuiya?
Jibu: Wasiwasi wangu mkubwa ni kuwa Jumuiya yetu watu hawaifahamu vizuri hivyo Serikali na wadau wote wa Afrika Mashariki wanapaswa wafanye kazi kubwa ya kuwaelimisha Watanzania kuhusu dhana nzima ya Afrika Mashariki.
Nia kubwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuinua hali za wananchi wa Afrika Mashariki. Kwa viwango vya dunia, wananchi wa Afrika Mashariki ni masikini sana na tunataka tupande na njia mojawapo ya kutuwezesha kupanda ni kuwa na masoko ya pamoja, kufanya biashara ya pamoja, kuzalisha kwa wingi, pamoja, msingi wa kuwa pamoja na msingi unaoeleweka kwa ajili ya maendeleo ya watu. Pia tunataka eneo letu liwe la kiushindani duniani, sasa hivi tuna mikataba mikubwa iankuja kutoka marekani wka mfano ya pamba, AGOA na kadhalika lakini tunashindwa kuitekeleza kama nchi mojamoja kwa sababu ya ule uwezo wetu na udogo wetu, kwa hivyo tukiunganisha nguvu pamoja, tunaweza tukanufaika zaidi.
Swali: Je ikiwa tutakapokuwa Shirikisho, ushiriki wetu katika jumuiya nyingine kama vile SADC na COMESA unakuwaje?
Jibu: Kuna misingi inayofuatwa duniani katika masuala ya mashirikiano. Mathalan haiwezekani kuwa katika Ushuru wa pamoja wa Forodha katika jumuiya zaidi ya moja. Hiyo ndiyo misingi ya kibiashara duniani iliyowekwa na World Trade Organization (WTO). Kwa hivyo ushirikiano wetu na jumuiya nyingine hauzuiliwi. Isipokuwa unaweza ukawa mdogo kwa mfano hatuwezi tukafanya ushirikano na SADC ambao unatuingiza katika Umoja wa Forodha wa SADC kama tayari tuko katika Umoja wa Forodha wa EAC. Sisi kama Afrika Mashariki tunaweza tukazingumza na wenzetu tukawaambia kwamba SADC ni muhimu kwa Afrika Mashariki, siyo muhimu kwa Tanzania peke yake, kwa hiyo tutafute namna ya kushirikiana na SADC kama Afrika Mashariki. Vivyo hivyo Kenya na Uganda nao wanaweza wakatushawishi kwamba COMESA ni muhimu siyo kwa Kenya na Uganda peke yake hata kwa Tanzania, hivyo tushauriane tutawezaje kushirikiana pamoja ndani ya COMESA. Kwa mfano kama sote tulio katika ushirikiano tutakubaliana tuingie SADC au COMESA kama Afrika Mashariki, haizuliwi.
Ninachosisitiza ni kwamba haya mambo ni mchakato, hakuna sababu ya kwenda haraka sana na hakuna sababu ya kwenda pole pole sana. Kusema kwamba tuingie katika Shirikisho 2013 ni pendekezo tu, kama Watanzania, Wakenya na Waganda wanataka iwe hivyo itakuwa hivyo lakini kama wananchi wa Afrika Mashariki hawataki iwe hivyo haiwezi kuwa hivyo.
Swali: Je nini uelewa wa wananchi wa Afrika Mashariki kuhusu Shirikisho?
Jibu: Wananchi wa Afrika Mashariki wanaelewa umuhimu wa kuingia katika Shirikisho na wanaelewa umuhimu wa kuwa na jumuiya yenye nguvu. Tatizo linakuja kwamba namna gani tufikie hapo? Bado kuna tofauti nyingi za kisheria na kisera katika nchi zetu. Kwa hiyo kazi kubwa ambayo nchi zinatakiwa ziifanye ni kuainisha sera kwa sababu sera zetu bado ziko tofauti sana. Tukiweza kuainisha sera zetu kwa haraka iwezekanavyo, ambao nadhani ndio msisitizo ungekuwapo hapo kwa sasa hivi, kwa kufanya hivyo kuungana itakuwa ni rahisi zaidi.
Wananchi wengi hawana hofu, hasa wale wa kawaida, isipokuwa ukienda kwa wasomi na wanasiasa wengi wanasita kwa sababu wanaangalia maslahi yao zaidi, je tukiungana nafasi zetu kama wanasiasa zitakuwaje? Lakini wananchi wa kawaida kama kweli jumuiya itawanufaisha, wao wako tayari. Hofu kubwa ya wananchi mathalan wa Tanzania yako katika ajira na ardhi.
Swali: Kwanini hofu ya Watanzania iko katika ajira?
Jibu: Mfumo wetu wa kielimu tuliokuwa nao toka mwanzo hautupi nafasi kubwa ya kuweza kuingia katika ushindani wa kiajira. Lakini hata hivyo mara nyingine hofu hayo haina mashiko sana, kwa sababu kuna Watanzania wengi wanaofanya kazi katika nchi mbalimbali, ukienda Lesotho, ukienda Botswana, Watanzania ndio wametamalaki katika taasisi za kielimu, kwa hiyo unaweza ukakuta watu wa Botswana wanawalalamikia Watanzania kama sisi tunavyowalalamikia Wakenya.
Lakini hatimaye watu wa Botswana wananufaika sana kwa sababu wanafunza vijana wao, baada ya miaka 20 au 30 ijayo watakuwa wameshafikia kiwango cha kujitosheleza na pengine hawatawahitaji tena Watanzania. Kwa hiyo hata Wakenya wakifurika Tanzania sasa hivi, hawatafurika milele, watakuwapo kwa muda fulani lakini baadaye watatuwezesha nasisi kujiwezesha kufikia kiwango hicho na kuboresha mifumo yetu.
Nadhani tusihofu sana kwa hilo, kwa sababu ni suala la wakati tu, Watanzania wako wengi, wanazaliana kila siku, watu milioni 30 kama ukimwi utaweza kudhibitiwa, nadhani tutafikia mahala tutaweza kushindana. Labda suala la msingi ni kwamba tupange vizuri sera zetu za elimu, hicho ndicho kitu cha msingi, lakini kuwa na hofu kwamba Wakenya watadhibiti ajira zetu si hofu ya msingi sana kwani hakuna mtu anayetaka kuhama Kenya kuja kuishi Tanzania, hata hapa Tanzania nani anapenda kutoka vijijini kuja kuishi mijini? Ni kwa sababu kuna tofauti, kama hakuna tofauti mtu anapenda kukaa alipo. Watu wengi sana wanaogopa kuhama, hata Wakenya nao wanaogopa kuhama, siyo kweli kama tukifungua milango leo, Wakenya watajaa. Watakuja wachache lakini hatimaye watarudi kwao.
Swali: Kwanini hofu iwepo katika masuala ya ardhi?
Nadhani tatizo lililopo Tanzania ni kuwa bado hatujajiweka sawa katika suala la ardhi. Ni vizuri tujiweke sawa na taratibu za kumiliki ardhi yetu. Hawa wageni wakija hawaibebi ardhi, wakiichukua wanakuja kuzalisha, kwanini tuwazuie? Tanzania kuna mapori tele, tuwaruhusu wayaendeleze ila tuweke vizuri sera zetu za kumiliki ardhi.
Mimi nadhani tunapaswa kuiweka nyumba yetu katika hali nzuri, (lets make our house in order) halafu tuwakaribishe wenzetu. Hatuna sababu kubwa ya kuhofia ardhi, kwa sababu zaidi ya asilimia 50 ya ardhi ya Tanzania iko katika hifadhi.
Swali: Dk. Nangale wewe ni mtunzi wa kitabu cha Politics of Partneship, kitu gani kilikusukuma kuandika kitabu hicho?
Jibu: Azma yangu ilikuwa ni kuweka wazi misingi ya ushirikiano. Nimejaribu kueleza mambo mengi ndani yake, nimejaribu kueleza jinsi gani taasisi na watu waliomo ndani ya taasisi, mahusiano yao yanaweza yakajenga au yakabomoa ushirikiano. Ushirikiano ni lazima uwe ni kitu cha kutoa na kuchukua. Dhana ya uhusiano ni ya muhimu sana katika kudumisha ushirikiano. Katika Afrika Mashariki tunayo bahati kwamba tuna uhusiano wa kihistoria, kwa sababu ukiangalia uhusiano wetu wa Afrika Mashariki kwa kweli ulikuzwa na mkoloni, mkoloni alijaribu kuziweka hizi nchi pamoja kwa manufaa yake, lakini ametutengeneza lugha ya Kiswahili kwa sababu lugha ya Kiswahili ni zao la mkoloni. Alijaribu kufanya mahusiano na watu wa Afrika Mashariki kwa kutumia ile lugha, kwa hiyo alichukua lugha yake, akachukua lugha za Waarabu, akachukua lugha za kibantu akaunda lugha maalum ya Kiswahili ambayo sasa hivi inatuunganisha sisi Watanzania na watu wa Afrika Mashariki.
Kama utakisoma kitabu hicho utagundua kwamba nazungumza kuhusu ushirikiano kwa filosofia zaidi, kwani ukweli ni kwamba tunaungana lakini wakati huo huo hatuungani. Kuna masuala ambayo tunajaribu kuunganisha yale ambayo tunafanana na tuna masuala ambayo kwa kweli hatuwezi tukayaunganisha kwa sababu za kihistoria na tofauti zetu. Ili muungano wetu uwezo kufanikiwa, lazima tukubaliane na tofauti zetu, kwamba tofauti zetu lazima zitaendelea kuwapo lakini kuungana tutaendelea kuungana. Wakenya watabaki Wakenya, Watanzania watabaki Watanzania, Waganda watabaki Waganda na kadhalika.
Swali: Je Umoja wa Afrika Mashariki utakuwa sawa na ule Umoja wa Ulaya (EU)?
Jibu: Umoja wa Ulaya si kigezo chetu, Ushirikiano wetu ni wa kipekee. Nchi za Ulaya hazijaungana mpaka leo, wamekubaliana mambo fulani fulani tu, katika masuala ya kijamii yaliyiozungumzwa katika mkataba wa Mostrich unaozungumzia masuala ya jamii, Uingereza na Denmark wamejitoa, Sarafu ya Pamoja, Uingereza na Denmark wamejitoa. Umoja wa Ulaya unashikiliwa na Ufaransa na Ujerumani lakini leo Ujerumani ikijitoa kwenye Euro, Euro itaanguka. Kwa hivyo sisi Afrika Mashariki tuna azma kubwa zaidi kuliko Umoja wa Ulaya, sisi sasa hivi tunafikiria kuunda ‘Supra State’ taifa la Afrika Mashariki, Ulaya hawajafikia hiyo hatua, wako mbali sana kufikia Taifa la Ulaya, wao wameungana katika mambo ya Ushuru wa Forodha na Soko la Pamoja lakini katika Shirikisho la kisiasa hawajafikia.
Swali: Je tutaweza kukabiliana na changamoto za Shirikisho ama Muungano?
Jibu: Watanzania tunao uzoefu wa miaka zaidi 40 ya Muungano, kwa hivyo Watanzania ni walimu wazuri sana kwa wenzetu kwamba Muungano au Shirikisho si kitu rahisi sana, majadiliano ya mara kwa mara na ya muda mrefu yanahitajika, ni kitu cha kujadiliana kwa miaka mingi, yaweza hata kufikia miaka 50 mnajadiliana tu kabla hamjafikia pale mnapopataka ama mliporidhiana.
Friday, January 26, 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment